JULIANA SIMON NEWS
Monday, June 6, 2016
Samia aagiza kuundwa kamati za mazingira
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza wananchi katika ngazi zote kuunda kamati ndogo za mazingira zitakazosimamia sheria ndogo za mazingira na utunzaji wa misitu ili kulinda na kuokoa vyanzo ya maji.
Amewataka wananchi kwa utashi wao kuhakikisha katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani wanashiriki kikamilifu katika kusimamia na kuhakikisha vyanzo vya maji vinahifadhiwa ili binadamu na wanyamapori waishi.
“Nielekeze kuwa, kamati za mazingira katika ngazi za vijiji, vitongoji, mitaa, kata na wilaya ambazo sheria ya mazingira imeelekeza ziwepo, zianzishwe au zifufuliwe na zichukue nafasi ya kutambua na kusimamia vyanzo vya maji vilivyopo,” alisisitiza Samia.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani yaliyofanyika duniani kote jana, alisema kazi nyingine ya kamati hizo ndogo ni kuhakikisha pia inafufua vyanzo vya maji vilivyoharibiwa kwa kuvihifadhi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Katika kuadhimisha siku hiyo nchini kaulimbiu ya Tanzania ni ‘tuhifadhi vyanzo vya maji kwa uhai wa taifa letu’. “Maji ni uhai wa viumbe vyote akiwemo binadamu, wanyamapori, mimea na ni uhai wa uchumi wa taifa.”
Kutokana na ukweli huo, Tanzania imeamua kuwa na kaulimbiu hiyo kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira hususan vyanzo vya maji kutokana na kukithiri kwa shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, uchimbaji wa madini na matumizi ya nishati.
Alisema hali hiyo imesababisha kuwepo na upungufu wa mtitiriko wa maji katika mito mingi nchini takribani kwa kipindi cha miongo mitano iliyopita na baadhi ya mito imebadilika na kuwa ya msimu, kuchafuliwa sana na mingine kukauka.
“Tukiendelea na mwenendo huu wa uharibifu wa vyanzo vya maji, mito yetu mikuu hapa nchini kama vile Rufiji, Pangani, Ruaha na mingineyo inayotegemewa sana kwa uhai na ustawi wa Watanzania wengi, itakauka ndani ya miaka 15 ijayo,” alisisitiza.
Akizungumzia maadhimisho ya siku hiyo duniani, alisema kimataifa yanaadhimishwa nchini Angola yakiwa yamebeba kaulimbiu ‘go wild for life save the environment’ inayokumbusha umuhimu wa kuchukua hatua za makusudi kulinda maisha ya wanyamapori.
Kihistoria siku ya mazingira ilianzia mwaka 1972 wakati Baraza la Umoja wa Mataifa lilipopitisha maamuzi ya kuanzishwa kwake kwenye mkutano wa kwanza wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo Endelevu uliofanyika jijini Stockholm nchini Sweden.
Friday, June 3, 2016
PATA ELIMU KUTOKA KIKUNDI CHA MAISHA YA THAMANI NDANI YA CHUO CHA UANDISHI WA HABARI NA UTANGAZAJI ARUSHA (AJTC)
Kikundi cha MAISHA YA THAMANI kinacholenga kutoa elimu kwa jamii ya kitanzania inayoratibiwa na Bw Fedinand Shayo, kinatoa elimu ya Maisha kwa wanafunzi wa chuo cha uandishi wa habari na utangazaji Arusha AJTC.
Mkurugenzi wa Mafunzo katika chuo cha uandishi wa habari na utangazaji Arusha.Bw Joseph Mayagila |
Mtangazaji wa Redio Five 5, Bw Godfrey Thomas akizungumza na wanafunzi wa AJTC |
Wanafunzi wa chuo cha Uandishi wa habari na utangazaji Arusha,Wakisikiliza mafunzo kutoka kwa wageni wao...MAISHA YA THAMANI |
Wakufunzi wa Chuo cha uandishi wa Habari na utangazaji Arusha Bw Andrea ngobole kutoka kushoto,na Mwl Elihuruma Chao ...kulia |
Mkufunzi wa AJTC Bw Andrea Ngobole akizungumza na wanafunzi kwenye Semina ya MAISHA YA THAMANI |
Bw Proti Profit Manga akitoa elimu ya maisha kwa wanafunzi wa AJTC |
Bi Hellen akitoa elimu kwa wanafunzi wa chuo cha Uandishi wa Habari na Utangazaji Arusha |
Bw Fedinand Shayo Mratibu wa MAISHA YA THAMANI. Picha na PPM Na RAYMOND WILLIAM |
MR&MRS ELIHURUMA CHAO
TUMTEGEMEE MUNGU KWA KILA JAMBO
KIKAO CHA KWANZA CHA BUNGE LA (AJTC) MASWALI NA MAJIBU NDANI YA UKUMBI WA CHUO HICHO
Kikao cha bunge la wanafunzi wa chuo cha uandishi wa habari kilichowakutanisha baadhi mawaziri
kutoka wizara tofauti tofauti kwa lengo la kuwasilisha ripoti na kujibu maswali ya wabunge hao.
Wizara ambazo zilitakiwa kuwasilisha ripoti zao ni wizara ya
Habari,fedha,wizara ya sheria na maadili pamoja na wizara ya afya ulinzi
na makazi.Kutokana na wingi wa maswali mengi kwa wizara ya habari
hivyo kupelekea wizara nyingine kutowasilisha
ripoti
Mh Elia Baraka naibu waziri wa Elimu akijibu maswali yaliyoulizwa na wabunge
Mawaziri na manaibu waziri wa wizara mbalimbali wakisubiri kutumbuliwa na wabunge
Thursday, June 2, 2016
TCRA iungwe mkono kuondoa simu feki
TANGU Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilipotoa tamko mwezi Desemba mwaka jana kuwa itazifungia simu feki, yamekuwapo malalamiko ya wananchi na wafanyabiashara, wanaotaka muda huo uongezwe.
Mpaka sasa zimebaki siku 13 tu kwa TCRA kuchukua hatua hiyo huku Watanzania wanaotumia simu hizo wakiwa asilimia 18 kutoka asilimia 40 ya awali, kabla ya tangazo hilo.
Kitu cha kushangaza ni kuwa wengi wanaodai kuongezewa muda ni wafanyabiashara, ambao wanataka wamalize kwanza mzigo wa simu feki walizoingiza kwa kuwauzia Watanzania, ambao hawatakiwi kuwa na simu feki.
Kifungu cha 84 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, kinataka kuwepo kwa mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa Vifaa vya Mawasiliano vya Mkononi, ambayo inatakiwa ihifadhiwe na kuendeshwa na TCRA.
Pia sheria hiyo inawataka watoa huduma wa mawasiliano, yanayotumia vifaa vya mkononi kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mkononi, vinavyotumika kwenye mitandao yao.
Kwa maana hiyo, kutakuwa na utambuzi wa kati ya mtumiaji wa simu na kifaa chake kwenye kampuni hizo, hivyo kutoa na fursa ya wananchi kuwa na matumzi sahihi ya simu, ikiwa tofauti na sasa.
Kwa muda sasa kumekuwapo na kilio cha wananchi ya kuibiwa fedha zao kupitia simu au kuibiwa simu zenyewe. Ili kuondokana na tatizo hilo, basi wakati umefika sasa kwa Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia TCRA ya kuondoa simu feki katika soko la Tanzania kwa manufaa ya wananchi.
Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa mfumo huu wa kielektroniki wa Rajisi, ambao utahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi, una lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhiviwango vya matumizi katika soko la mawasiliano.
Endapo mtu atapigiwa simu na kutapeliwa fedha, mfumo huo utaweza kutambua namba tambulishi ya simu ambayo imetumika na mtu aliyeisajili. Ni rahisi kufuatilia mtu mwenye simu halisi na ni ngumu kwa mtu mwenye simu feki.
Pia mfumo huo utasaidia kuondoa tatizo la wizi wa simu, kwani mtu aliyeibiwa akitoa taarifa za kupotelewa kwa simu yake, simu hiyo itafungwa ; na ikishafungwa haitaweza kutumika na mtandao wowote wa simu hapa nchini, kwa maana nyingine aliyenunua simu hiyo ya wizi atabaki na ‘toy’ Pia hatua hiyo itahimiza utii wa sheria, kwani Kifungu cha 128 cha EPOCA kinachomtaka mtumiaji wa simu, kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu na Kifungu cha 134 cha Sheria hiyo, kinachotaka kampuni za simu kutotoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa, kama ilivyoelezwa hapo juu.
Mteja anapopoteza tu simu yake ya kiganjani, anatakiwa kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha karibu, ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio, maarufu kama RB na kuipeleka kwa mtoa huduma, ambaye baada ya kuhakiki, ataifungia simu hiyo isitumike kwenye mitandao mingine ya simu.
Hivyo Mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa Vifaa vya Mawasiliano vya Mkononi, una lengo la kuwahakikishia watumiaji usalama wakati wanapotumia vifaa hivyo vya mawasiliano, vikiwemo simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tabuleti). Ni vyema watumiaji wa simu na vifaa vingine vya mawasiliano, kuunga mkono juhudi hizo kukomesha tatizo ili kuimarisha usalama wetu.
Tuesday, May 31, 2016
VIJANA NCHINI WASHAURIWA KUJIUNGA NA MASHIRIKA YA KUJITOLEA ILI WAJIONGEZEE UJUZI NA MAARIFA
Vijana nchini Tanzania wameshauriwa kuwa tayari kufanya kazi kwa kujitolea ili kujiongezea ujuzi, uwezo, maarifa na kuleta mabadiliko katika jamii zao,hayo yalielezwa na Meneja wa Maendeleo ya Vijana wa shirika la Raleigh Tanzania, Genos Martin wakati wa mahojiano maalum na mwandishi wa habari hii.
Martin alisema kuwa ni vyema kwa vijana kujiunga na mashirika ya kitaifa na ya kimataifa ya kujitolea kwani kwa kufanya hivyo kutawapa vijana fursa ya kuongeza ujuzi na maarifa ambao utawasaidia katika sehemu mbalimbali.
Martin alisema, “Kufanya kazi kwa kujitolea ni kitu kigeni nchini kwetu tofauti na Mataifa ya nchi zilizoendelea, watu waliowahi jitolea wanapewa kipaumbele kwenye maombi ya kazi tofauti na nchini kwetu. Hii inafanya kujitolea kuwa jambo la muhimu sana kwenye mataifa ya wenzetu”
“Vijana wengi wanalalamika kuwa nafasi nyingi za kazi zinawataka wawe na uzoefu wa miaka mitatu nakuendelea, hawajui ni vipi wanaweza kupata uzoefu lakini kama wakijiunga na haya mashirika ya kujitolea wanaweza pata huo uzoefu na kuwafanya wawe na nafasi nzuri pindi waombapo ajira” aliongezea Martin.
Aidha, Afisa Mawasiliano wa Raleigh Tanzania, Kennedy Mmari alieleza kuwa ni kawaida ya shirika hilo kutafuta vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini ambao huungana na vijana wenzao kutoka mataifa ya mbali mbali ya Ulaya na Amerika.
Mmari aliongezea, “Raleigh tuna programu kwa vijana zinazohusu ujasiriamali, usafi, maji na utunzaji wa mazingira, kijana yeyote anaweza kujjiunga nasi na kufanya program zetu. Hatutoi malipo yoyote wala hawatulipi chochote isipokuwa tunagharamia mahitaji yao yote ya msingi pindi wakiwa kwenye programu”
Wanafunzi wa shule ya Msingi Chibe iliyopo kata ya Old Shinyanga mkoani Shinyanga wakishuhudia ufunguzi wa kituo cha elimu ya awali kilichojengwa na na vijana wa kujitolea kwa msaada wa shirika la Raleigh Tanzania.
Kwa upande wa vijana waliofanya programu na shirika hilo wameshukuru kwa nafasi waliyopewa kwani imewasaidia kupata ujuzi na ufahamu wa mambo tofauti ikiwemo jinsi ya kuandaa na kusiammia biashara.
Mmoja wa vijana ambao wamepata fursa hiyo, Sia Malamsha, alisema kuwa anajiona wa tofauti baada ya kumaliza programu, hakuwahi fikiria kama kuna watu Tanznaia hawana huduma za maji safi na salama lakini kupitia programu za Raleigh nimeweza fika kwenye jamii hizo na kuwasaidia kutatua matatizo hayo.
“Nimekuwa sehemu ya mabadiliko makubwa katika nchi yangu, najivunia kuona nimefanya kitu kuikomboa jamii ya Watanzania” aliongezea Bi. Malamsha.
Vijana wa Shirika la kujitolea la Raleigh wakishiriki ujenzi wa choo katika moja ya miradi yao
Naye kijana Ashiru Said aliyefanya programu ya ujasiriamali amesema kua programu za Raleigh zimemsaidia kupata elimu ya kusimamia na kuendesha biashara.
“Nimeweza kupata elimu ya ujasiriamali, baada ya kurudi nyumbani jamii imefaidika na elimu niliyoipata kwani nimeweza waelimisha vijana wenzangu jinsi ya kuanzisha na kusimamia biashara zao wenyewe” alimalizia Said.
Raleigh Tanzania ni shirika lisilo la kiserikali lenye ofisi zake mkoani Morogoro na kufanya programu za kujitolea kwa lengo la kuisaidia jamii ya Tanzania sehemu mbalimbali.(P.T)
Subscribe to:
Posts (Atom)