TANGU Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilipotoa tamko mwezi Desemba mwaka jana kuwa itazifungia simu feki, yamekuwapo malalamiko ya wananchi na wafanyabiashara, wanaotaka muda huo uongezwe.
Mpaka sasa zimebaki siku 13 tu kwa TCRA kuchukua hatua hiyo huku Watanzania wanaotumia simu hizo wakiwa asilimia 18 kutoka asilimia 40 ya awali, kabla ya tangazo hilo.
Kitu cha kushangaza ni kuwa wengi wanaodai kuongezewa muda ni wafanyabiashara, ambao wanataka wamalize kwanza mzigo wa simu feki walizoingiza kwa kuwauzia Watanzania, ambao hawatakiwi kuwa na simu feki.
Kifungu cha 84 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010, kinataka kuwepo kwa mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa Vifaa vya Mawasiliano vya Mkononi, ambayo inatakiwa ihifadhiwe na kuendeshwa na TCRA.
Pia sheria hiyo inawataka watoa huduma wa mawasiliano, yanayotumia vifaa vya mkononi kuweka mfumo wa kudumu wa kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mkononi, vinavyotumika kwenye mitandao yao.
Kwa maana hiyo, kutakuwa na utambuzi wa kati ya mtumiaji wa simu na kifaa chake kwenye kampuni hizo, hivyo kutoa na fursa ya wananchi kuwa na matumzi sahihi ya simu, ikiwa tofauti na sasa.
Kwa muda sasa kumekuwapo na kilio cha wananchi ya kuibiwa fedha zao kupitia simu au kuibiwa simu zenyewe. Ili kuondokana na tatizo hilo, basi wakati umefika sasa kwa Watanzania kuunga mkono juhudi za Serikali kupitia TCRA ya kuondoa simu feki katika soko la Tanzania kwa manufaa ya wananchi.
Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa mfumo huu wa kielektroniki wa Rajisi, ambao utahifadhi kumbukumbu za namba tambulishi za vifaa vya mawasiliano vya mkononi, una lengo la kufuatilia namba tambulishi za vifaa vinavyoibiwa, kuharibika, kupotea au ambavyo havikidhiviwango vya matumizi katika soko la mawasiliano.
Endapo mtu atapigiwa simu na kutapeliwa fedha, mfumo huo utaweza kutambua namba tambulishi ya simu ambayo imetumika na mtu aliyeisajili. Ni rahisi kufuatilia mtu mwenye simu halisi na ni ngumu kwa mtu mwenye simu feki.
Pia mfumo huo utasaidia kuondoa tatizo la wizi wa simu, kwani mtu aliyeibiwa akitoa taarifa za kupotelewa kwa simu yake, simu hiyo itafungwa ; na ikishafungwa haitaweza kutumika na mtandao wowote wa simu hapa nchini, kwa maana nyingine aliyenunua simu hiyo ya wizi atabaki na ‘toy’ Pia hatua hiyo itahimiza utii wa sheria, kwani Kifungu cha 128 cha EPOCA kinachomtaka mtumiaji wa simu, kutoa taarifa ya kupotea au kuibiwa kwa simu au laini ya simu na Kifungu cha 134 cha Sheria hiyo, kinachotaka kampuni za simu kutotoa huduma kwa simu ambayo imefungiwa, kama ilivyoelezwa hapo juu.
Mteja anapopoteza tu simu yake ya kiganjani, anatakiwa kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha karibu, ambapo atapewa namba ya kumbukumbu ya taarifa ya tukio, maarufu kama RB na kuipeleka kwa mtoa huduma, ambaye baada ya kuhakiki, ataifungia simu hiyo isitumike kwenye mitandao mingine ya simu.
Hivyo Mfumo wa Rajisi ya Namba za Utambulisho wa Vifaa vya Mawasiliano vya Mkononi, una lengo la kuwahakikishia watumiaji usalama wakati wanapotumia vifaa hivyo vya mawasiliano, vikiwemo simu za kiganjani na vifaa vya mawasiliano vya kiganjani (tabuleti). Ni vyema watumiaji wa simu na vifaa vingine vya mawasiliano, kuunga mkono juhudi hizo kukomesha tatizo ili kuimarisha usalama wetu.
No comments:
Post a Comment