RAIS John Magufuli hivi karibuni alitengua uteuzi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango na Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), Abdul Dachi kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kuhusu idadi ya watumishi hewa wa mkoa huo.
Kilango alidumu katika utumishi wa umma akiwa mkuu wa mkoa huo kwa siku 28 tu, tangu alipoapishwa Machi 15 mwaka huu. Rais alisema Kilango alitoa taarifa za kuwa mkoa huo, hauna watumishi hewa.
Hivyo, alichofanya yeye ni kutuma timu ya ukaguzi, iliyokwenda kufanya uchunguzi, ambapo hadi kufikia Aprili 10, mwaka huu ilibaini kuwepo watumishi hewa 45 huku uhakiki ulikuwa ukiendelea katika wilaya mbili za Ushetu na Shinyanga Vijijini.
Rais alisema watumishi hewa waliobainika, walikuwa tayari wameshalipwa Sh milioni 339.9. Hadi juzi wafanyakazi hewa waliokuwa wamegundulika tayari katika mkoa huo walikuwa 226.
Kutokana na hali hiyo, Rais aliwataka wakuu wa mikoa yote, wawafichue watumishi hewa wote ili waondolewe mara moja. Pia, aliagiza timu iliyofanya uchunguzi mkoani Shinyanga, itumike kufanya uchunguzi katika mikoa mingine kwa lengo la kukomesha upotevu mkubwa wa fedha za umma, kwani mpaka kufikia Machi 31 mwaka huu jumla ya watumishi hewa 5,507 walibainika.
Imeelezwa kuwa Sh bilioni 583 ambazo serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kulipa mishahara, Sh bilioni 54 zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa mishahara ya watumishi hewa. Hatua ya Rais kutengua uteuzi huo wa Kilango, imepokewa kwa hisia tofauti na wananchi wengi. Wengine wamepongeza na wengine wameona angepewa muda kwa kupewa onyo ili kuendelea kuhakiki.
Lakini ni dhahiri kuwa uamuzi huo wa Rais, una lengo la kutaka wakuu wa mikoa na watendaji wengine, kufanya kazi kwa vitendo; na siyo kusubiri kupelekewa taarifa, ambazo inakuwa rais kudanganywa.
Katika kuhakikisha azma ya Rais inafanikiwa kuondoa watumishi hewa serikalini na kuwa historia, ni vema timu ya uhakiki kupita mikoa yote, kama walivyoagizwa na rais, kwani lililotokea Shinyanga, linaweza kutokea katika mkoa mwingine wowote.
Timu ya uhakiki itabaini pia kama kuna walioonewa kwa sababu mbalimbali na pia itaangalia kama wakuu wa mikoa, hawakuweza kubaini watumishi nwengine. Inawezekana ikachukua muda mrefu kufanya uhakiki kwa mara ya pili.
Lakini, jambo lolote jema ni lazima lifanywe hata mara tatu ili kuondoa shaka na mwanya wowote, utakaosababisha watumishi hewa wajirudie wakati mwingine. Hakuna ubishi kuwa fedha nyingi zilizolipwa kwa watumishi hewa, zingeweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo na kuwaondolea wananchi kero mbalimbali katika jamii, kama ubovu wa barabara na upungufu wa madarasa na madawati shuleni.
Hivyo jitihada za Rais katika kudhibiti watumishi hewa, zinapaswa kuungwa mkono na watanzania wote, hususan watumishi wa idara zinazohusika na malipo, kwani wao ni rahisi kujua kama mtu ameacha kazi, amestaafu, yupo masomoni au amekufa.
Naomba watendaji katika mikoa yote, kutoa taarifa za haraka na kwa uhakika kabla ya timu ya uhakiki haijafika. Wale waliodanganya katika uhakiki wa watumishi hewa, wachukuliwe hatua kali, kwani lazima walidanganya huku wakifahamu ukweli.