Wednesday, April 13, 2016

Wasiwasi juu ya mifuko ya jamii upatiwe majibu


HIVI karibuni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), iliwaweka kitimoto Mawaziri, Gavana wa Benki Kuu (BoT) na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), kutokana na kutoridhishwa na hali ndani ya mifuko ya jamii.
Katika kikao hicho, wabunge walieleza kusikitishwa na hali ilivyo ndani ya Mfuko wa Pensheni wa Watumishi wa Umma (PSPF), hatua inayotishia uhai wake. Aidha, wabunge pia walisikitishwa na hali ilivyo ndani ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), lakini pia hivi karibuni kumekuwepo kwa tetesi za hali kutokuwa nzuri sana ndani ya Mfuko wa Pensheni wa Mashirika ya Umma (PPF).
Mawaziri walioitwa mbele ya kamati hiyo ni wa Fedha na Mipango, ambaye aliwakilishwa na Naibu Waziri, Dk Ashatu Kijaji, Waziri wa Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, ambaye aliwakilishwa na Naibu Waziri, Antony Mavunde na SSRA iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu, Irene Isaka.
Kupitia kikao hicho, wabunge walisema Mfuko wa PSPF upo katika hatari ya kufa kutokana na kukabiliwa na nakisi kubwa ya kifedha, hatua inayofanya ushindwe kulipa mafao ya wastaafu wa Serikali, hususan walimu, kwa muda mrefu sasa.
Watunga sera hao walisema, mfuko huo umepoteza uwezo wa kulipa mafao, kutokana na fedha za wastaafu zilizokuwepo kukopwa na Serikali, na kwamba chombo hicho kilishindwa kuwasilisha michango ya makato kuanzia Septemba mwaka jana hadi Februari mwaka huu, ambayo ni Sh bil 989.7.
Walisema, hadi sasa walimu wastaafu 1,038 hawajalipwa mafao yanayofikia Sh bil 53.64, huku wengine 381 wakidai mafao ya vifo ya Sh bilioni tano. Mbali ya hao, wabunge walisema wapo wastaafu wengine 3,016 kutoka sekta nyingine wanaoidai PSPF mafao yanayofikia Sh bil 29.90 na wengine 259 ambao si walimu,wakiudai mfuko huo Sh bil 2.7 za mafao ya vifo bila kulipwa kwa muda mrefu.
Mbali ya madai hayo, walisema pia kuwa, PSPF kwa muda mrefu imeshindwa kulipa mafao ya mikopo ya walimu 307 ya Sh bil 8.67 na wadaiwa wengine 200 wa sekta nyingine ambao madeni yao kwa mfuko huo wa PSPF hadi sasa yamefikia Sh bil 8.25.
Walisema, kiashiria kikubwa kinachotoa ishara kwamba Mfuko wa PSPF unakaribia kufa ni kutokana na kuwepo kwa hundi 11,014 ambazo zipo tayari kwa ajili ya kulipwa zikiwa zimekamilika katika kila eneo zenye thamani ya Sh bil 166.68, lakini wastaafu hawajakabidhiwa hundi hizo kwa vile fedha za kuwalipa hazipo.
Kuhusu Shirika la NSSF, wabunge walisema wanashangazwa na hatua ya shirika hilo kuendelea kutajwa kwa mabaya, ikiwemo ubadhirifu mkubwa wa fedha na uwekezaji mbovu, bila SSRA kutoa taarifa ya ufafanuzi.
Walisema kwa muda mrefu sasa, baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti kwamba hali si shwari ndani ya NSSF vikidai kuwepo kwa ufisadi wa mabilioni ya fedha, unaofanywa na uongozi wa shirika, lakini pia uwekezaji usio na tija, hatua ambayo inasababisha picha mbaya na kuwakatisha tamaa wachangiaji.
Wabunge walihoji; “Hivi inakuwaje mambo kama haya yanazungumzwa halafu Mdhibiti (SSRA) upo kimya? Wizara husika (Fedha na Mipango) ipo kimya? Hatua hii inaweza kusababisha wachangiaji kuhama au hata picha ya Mfuko kuchafuka.
Kama vile hiyo haitoshi, hivi karibuni vyombo mbalimbali vya habari pamoja na mitandao ya kijamii vimeanza kuripoti taarifa za kuwepo kwa njama za kuihujumu PPF huku wakitoa taarifa mbalimbali za kuwepo kwa ufisadi ndani ya Mfuko huo.
Ninaungana na wabunge kwa kuandika Wazo hili, ili mamlaka husika na hasa SSRA iweze kutoa taarifa za kina na za kimchanganuo kuonesha hali ilivyo ndani ya mifuko hii kutokana na ukweli kwamba, wachangiaji wake wameanza kupata shaka na wasiwasi kuhusu usalama wa fedha wanazochangia.

No comments:

Post a Comment