Monday, April 25, 2016

Ataka wanaomkejeli Magufuli wachunguzwe


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Rorya mkoani Mara kimesema watu wanaokejeli juhudi zinazofanywa na Rais John Magufuli si wazalendo , wanapaswa kuchunguzwa na Serikali.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Samwel Kiboye alisema hayo jana jijini Mwanza alipokuwa akizungumzia juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli kuchukua hatua dhidi ya watu wanaoiba fedha za umma.
“Kumeibuka tabia chafu kutoka kwa baadhi ya watu nchini kwa sasa, wanapotosha wananchi juu ya kazi nzuri inayofanywa na Rais Magufuli katika kuwashughulikia mafisadi na wanaoiba rasilimali za nchi, ”alisema.
Alisema taifa haliwezi kukubali kuona kazi nzuri inayofanywa na Rais ikipotoshwa na watu wachache aliosema hawaitakii mema nchi. “Nani haoni kazi kubwa inayofanywa na Rais ..., ameimarisha ukusanyaji wa mapato na ameboresha sekta ya afya, miundombinu, hivi watu hawa wanataka Rais awafanyie nini?,” alihoji na kuongeza:
“Ni aibu kuona watu wanahoji mambo ambayo hata kwa mtu ambaye hakwenda shule anaona mafanikio makubwa aliyofanya Rais Magufuli katika kipindi kifupi ambacho amekuwa madarakani.”
“Huko nyuma walikuwa wanamlaumu aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete kuwa alikuwa mpole, leo tumempata Rais anayesimamia ukuaji wa uchumi wa nchi wanaleta siasa, sisi Rorya tunasema tuko imara na tutakufa na Rais Magufuli”.
Aliwataka wakuu wa wilaya na mikoa nchini kuanza mkakati wa kuwashughulikia watu wanaomjadili Rais kwa lengo la kupinga mafanikio ya serikali ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Katika hatua nyingine, Kiboye alisema CCM wilayani humo inaanza kuwashughulikia makatibu wa CCM wa Kata ambao ni majipu wanaoanza kuiba fedha za chama. “Kuna baadhi ya watendaji wabovu katika chama wameanza kuonekana kuiba fedha za makatibu wa tawi, hawa nao ni majipu muda ukifika tutawatumbua”, alisema

No comments:

Post a Comment