WATANZANIA jana waliadhimisha miaka 52 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, huku Rais John Magufuli akifuta sherehe za siku hiyo na kutaka kila Mtanzania aitumie kwa shughuli za uzalishaji mali, huku yeye akiitumia kufanya kazi kwa kuendesha kikao na watendaji mbalimbali wa serikali, kilichozaa utumbuaji wa majipu katika Mamlaka ya Usimamizi wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Dk Magufuli ameivunja Bodi ya TCRA na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dk Ally Simba kutokana na kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa mawasiliano ya simu (TTMS) na kusababisha nchi kupoteza mapato ya takriban Sh bilioni 400 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli alichukua hatua hiyo jana Ikulu Jijini Dar es Salaam baada ya kufanya kikao cha kazi kati yake na viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Wizara ya Fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Kwa mujibu wa Ikulu, Machi 22, 2013 TCRA iliingia mkataba na Kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa mapato ya simu, ambao kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano, lakini mpaka sasa SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo, kinachohusu udhibiti wa mapato ya simu za ndani (offnet), hali ambayo imesababisha serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa Sh bilioni 400 kwa mwaka.
Pamoja na kuivunja Bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Simba, Rais Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo mara moja.
Aidha, Rais Magufuli amewataka Profesa Mbarawa, Katibu Mkuu na Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani uanze kufanya kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.
Kwa mujibu wa Ikulu, Rais Magufuli amesisitiza, “Waziri hakikisha unachukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato yote ya serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayekwamisha jambo hili.”
Katika ripoti yake ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2014/15 aliyoiwasilisha juzi bungeni, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad alisema TCRA inaendesha mfumo wa udhibiti wa mawasiliano ya simu (TTMS) unaofuatilia mwenendo wa mawasiliano ya simu kutoka kwa watoa huduma za mawasiliano waliopewa leseni.
Alisema mfumo huo wa mawasiliano, kwa sasa unaweza kudhibiti mapato yatokanayo na mawasiliano ya kimataifa na haujaweza kudhibiti mapato yatokanayo na mawasiliano ya ndani.
Aidha, alisema kukosekana kwa mawasiliano ya kutosha kati ya taasisi muhimu zinazoweza kunufaika na mtambo huo, kama vile Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kumesababisha serikali kuendelea kupoteza mapato yatokanayo na mawasiliano ya simu za ndani.
Alisema pia amebaini kukosekana kwa usimamizi wa gharama za simu wakati wa kutuma na kupokea fedha kupitia kampuni za simu (mobile money banking) kwa BoT na TRA.
Katika mapendekezo yake kuhusu TCRA, Profesa Assad alisema upo umuhimu wa kuunganisha TRA katika mfumo huo na kuhakikisha kuwa usimamizi kupitia mamlaka husika kwa maana ya BoT na TRA unaimarishwa ili kuongeza udhibiti wa mapato unaotokana na mawasiliano ya ndani na nje ya nchi.
Dk Simba aliteuliwa na Profesa Mbarawa, Julai 6, 2015 kwa kipindi cha miaka mitano, akichukua nafasi ya Profesa John Nkoma aliyestaafu. Dk Simba ana uzoefu wa zaidi ya miaka 16 katika sekta ya mawasiliano, ambayo amefanya kazi kwa watoa huduma, taaluma ya utafiti, udhibiti pamoja na Serikali Kuu. Kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2013, alifanya kazi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kama Meneja Mipango na Utafiti wa Mamlaka.
No comments:
Post a Comment