Monday, April 25, 2016

Tanapa yatoa milioni 86/- kujenga makazi ya polisi



SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limetoa Sh milioni 86 kwa ajili ya kujenga nyumba ya askari wa kituo cha Polisi kilichopo kata ya Idodi wilayani Iringa mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana waliofika kata hiyo ya Idodi kwa ajili ya kujionea miradi ya ujirani mwema inayofadhiliwa na Tanapa, Mkuu wa Kituo cha Polisi Idodi, Dennis Mgaya alishukuru kwa ujenzi wa nyumba hiyo. Hata hivyo alisema bado wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa kituo cha Polisi.
Alisema polisi hao wanatumia vyumba sita vilivyopo ndani ya nyumba hiyo iliyogawanywa mara mbili. “Licha ya changamoto ya kituo cha Polisi cha kisasa lakini tunashukuru Tanapa kwa kutujengea nyumba ya polisi kutokana na mradi wa ujirani mwema hivyo tunaomba kituo cha Polisi cha kisasa zaidi “.
Pia aliongeza kuwa hivi sasa polisi hao wanatumia ofisi waliyopewa na Mtendaji wa Kata ya Idodi, Ignas Kwangulilo kama kituo cha Polisi cha Idodi. Mhifadhi wa ujirani mwema wa Ruaha, Wilbroad Mamuya alisema hifadhi hiyo inashirikiana na wananchi kuleta maendeleo kwa wanavijiji 64 wanaozunguka hifadhi hiyo ya Ruaha.
Diwani wa Kata ya Idodi, Onesmo Mtatifikolo alisema wanashirikiana vyema na Hifadhi ya Taifa Ruaha katika kujikwamua kiuchumi kwa wananchi ikiwemo suala la elimu kwani pia wamejenga darasa moja shule ya msingi Tungamalenga lililogharimu Sh milioni 44.2.

No comments:

Post a Comment