MKAAZI wa kijiji cha Chamboni Shehia ya Wilaya ya Micheweni Pemba Bakar Haji Faki (20) amekutwa akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba ndani ya nyumba yake anayoishi .
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo walisema limetokea usiku wa Jumatano majira ya saa tatu , ambapo walimkuta akiwa amejitundika na tayari amefariki dunia .
Ali Massoud Kombo Mkaazi wa Micheweni aliliambia Gazeti hili kwamba tukio limeshangaza wengi kwani kabla ya kifo hicho kijana huyo hakuwahi kusumbuliwa na chembe za ugonjwa .
“Ni tukio ambalo limetushangaza vijana wengi ,kwani kijana mwenzetu hakukuwa na taarifa yoyote ya kusumbuliwa na ugonjwa wowote ”alifahamisha Ali Massoud Kombo .
Naye Kai Daud akizungumzia kifo hicho alisema kwamba kiliwashitua kwani kabla ya kutokea walikuwa pamoja na marehemu katika vijiwe /maskani zao wakijadili masuala ya kujipatia kipato .
Alisema kimetokea hatuna budi kushukuru kwani itakuwa ni mipango ya Mungu , kilicho baki na kumuombea mwenzetu ambaye tayari ametutangulia .
Tukio hilo pia limethibitishwa na kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Pemba Kamshina Msaidizi Mwandamizi Hassan Nassir Ali na kusema kwamba uchunguzi bado unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo hicho .
Alisema kwamba uchunguzi wa awali umethibitisha kwamba kijana huyo amefariki kwa kijitundika ndani ya nyumba (geto) yake ya kuishi na alionekana na jamaa zake akiwa tayari amefariki dunia .
“Ni kweli hili tukio limetokea na jeshi la Polisi bado linaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini hasa nini chanzo cha kifo hicho , lakini uchunguzi wa awali umebaini kwamba amejinyonga kwa kutumia kamba ”alifahamisha.
Hata hivyo kamanda Nassir alisema ni vyema wananchi kujenga utaratibu wa kutafuta ushauri juu ya mambo ambayo yanawatatiza , kwani sio vizuri kuchukua maamuzi ya kuidhulumu nafsi .
No comments:
Post a Comment