Wednesday, February 24, 2016

Dk Kalemani atangaza neema kwa watumiaji umeme mdogo


Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani akionesha Kifaa cha ‘Lead Board’ kwa viongozi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma (hawapo pichani) hivi karibuni. Dk Kalemani alikutana na viongozi hao wakati wa ziara yake wilayani humo kukagua miradi ya umeme inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba.
Fundi Umeme, akifunga umeme wa REA kama alivyokutwa na Msafara wa Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, eneo la Buselesele mkoani Geita hivi karibuni. Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya kazi kukagua miradi ya umeme vijijini.

Na Veronica Simba - Kakonko

Serikali imesema, wananchi wa kipato cha chini, hususan wa vijijini, wenye nyumba zenye kuanzia Chumba kimoja hadi Vinne, wataunganishiwa umeme pasipo kutandaza nyaya za umeme (wiring) kwenye nyumba zao.

Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani, aliyasema hayo hivi karibuni Wilayani Kakonko, mkoani Kigoma, akiwa katika ziara ya kazi mkoani humo, kukagua miradi inayotekelezwa chini ya wizara yake, hususan ya umeme vijijini, kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Dk Kalemani alisema, badala ya kutandaza nyaya za umeme katika nyumba zao, wananchi hao watafungiwa kifaa maalum kijulikanacho kitaalam kama ‘Lead Board’, kitakachowawezesha kutumia umeme kama kawaida.

Alisema, utumiaji wa kifaa hicho ni teknolojia mpya itakayowasaidia wananchi wa kipato cha chini kuondokana na gharama kubwa za kutandaza nyaya ndani ya nyumba, ambazo mara nyingi husababisha wengi wao kushindwa kumudu gharama hizo na hivyo kukosa huduma muhimu ya umeme.

Hata hivyo, Dk Kalemani aliweka bayana kuwa, watakaonufaika na huduma hiyo ni wale tu wenye kipato cha chini, wanaomiliki nyumba ndogo za kuanzia chumba kimoja hadi vinne. “Wenye nyumba kubwa wataendelea na utaratibu wa kawaida wa kutandaza nyaya.”

Alisema, Serikali imefikia uamuzi huo, baada ya kuona wananchi wengi wa vijijini, ambao kipato chao ni duni, wanashindwa kunufaika na huduma ya umeme, licha ya Serikali kuwapelekea huduma hiyo kwa gharama nafuu sana kupitia Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa na REA.

"Kama Serikali, tumedhamiria kuhakikisha asilimia 75 ya Watanzania wanatumia nishati ya umeme ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia malengo hayo, ni lazima tuhakikishe tunawapatia huduma hiyo muhimu Watanzania wengi zaidi, na tuhakikishe wanawezeshwa kuitumia, hususani walioko vijijini, ambao wengi wao wana kipato cha chini,” alisisitiza Naibu Waziri.

Akifafanua zaidi kuhusu faida za kutumia kifaa hicho, Naibu Waziri alisema, wananchi watakaofungiwa ‘Lead Board’, watatumia shilingi 27,000 hadi 30,000 tu. Gharama hiyo inahusisha uwekaji wa nguzo, kuunganishiwa umeme nyumbani pamoja na kifaa husika.

Alibainisha kuwa, kimsingi, umeme wa REA ni bure, isipokuwa mwananchi analazimika kulipia shilingi 27,000 tu kama tozo ya kodi ya Serikali (VAT). “Tofauti na kulipia VAT, hakuna malipo hata Thumni kwani Serikali imegharamia umeme huo.”

Aliongeza kuwa, Serikali inaangalia utaratibu wa kuondoa hata shilingi 6,000 inayotumika kulipia fomu kwa ajili ya maombi ya umeme kama njia ya kumwezesha mwananchi wa kipato cha chini kutumia huduma hiyo.

Akizungumzia gharama za matumizi ya umeme, Dk Kalemani alisema, watumiaji wote wa umeme, ambao matumizi yao ni chini ya uniti 75, wanapaswa kulipia shilingi 100 tu za kitanzania kwa kila uniti moja. Alisema, gharama hiyo ni nafuu sana, hivyo hakuna sababu ya wananchi wa kipato cha chini kushindwa kutumia umeme kwani wako katika kundi hilo linalotumia umeme kidogo.

Dk Kalemani alifafanua kuwa, wapo baadhi ya wananchi wanaotumia umeme chini ya uniti 75, lakini kwa bahati mbaya, wamewekwa katika kundi la watumiaji wakubwa wa umeme, hivyo wanapaswa kupeleka malalamiko katika Ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika maeneo yao ili wabadilishwe na kurudishwa katika kundi wanalostahili kuwa.

Vilevile, aliwataka viongozi katika ngazi mbalimbali, kuanzia Kijiji hadi Mkoa, kuelimisha wananchi juu ya matumizi bora ya umeme, kwani wengi wanatumia umeme vibaya na hivyo kulazimika kulipia bili kubwa.

Akizungumzia suala la kukatika-katika kwa umeme, Dk Kalemani alisema, Wizara yake imewaagiza Mameneja wa Tanesco wa Wilaya, Mkoa na Kanda nchi nzima, kuhakikisha wanarekebisha miundombinu mibovu ya umeme kama vile nguzo na transfoma ili kutatua tatizo hilo.

“Kwa hiyo, kukatika-katika kwa umeme kunakotokana na masuala ya kibinadamu, hakutarajiwi kuendelea baada ya Machi 31, mwaka huu.”

Aidha, aliwataka viongozi katika ngazi za Vijiji, Tarafa, Wilaya na hata Mkoa, kuhakikisha wanawasilisha majina ya vijiji ambavyo havikupangwa kupelekewa huduma ya umeme katika Mradi wa REA Awamu ya II, unaotarajia kukamilika ifikapo mwezi Juni mwaka huu, ili viingizwe katika Mradi wa REA Awamu ya III, unaotarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu.

Alisisitiza kutokusahau maeneo muhimu kama Vituo vya Afya, Shule, Masoko, Magereza, Jeshi na mengine ya aina hiyo, ambavyo havikupangwa kwenye REA Awamu ya II, ili viingie katika REA Awamu ya III.

No comments:

Post a Comment