Kufuatia kukiuka sheria za utunzaji mazingira katika sehemu za kazi Naibu waziri ofisi ya makamu wa Rais muungano na mazingira Luhaga Mpina amekipa siku saba kiwanda cha A to Z kilichopo mkoani Arusha kulipa adhabu ya faini ya shilingi million sabini,na kuongeza kuwa kutokulipwa kwa gharama hiyo kutasababisha kiwanda hicho kufungwa.
Akiwa jijini Arusha Naibu Waziri ofisi ya makamu ya rais muungano na mazingira ametembelea soko kuu pamoja na eneo la machinjio na baadae kuelekea katika maeneo ya viwanda .
Akiwa katika kiwanda cha kutengeneza nguo na bidhaa za plastiki cha A to Z Naibu Waziri aliyeambatana na wataalamu wa mazingira wamefanya ukaguzi katika kiwanda hicho na baadae katika maelezo yake ndipo ilipobainika kuwa kiwanda kilipewa adhabu ya kulipa shilingi million sabini iliyotolewa mwishoni mwa mwaka jana kwa ni kosa la kukiuka sheria ya mazingira ambayo mpaka hivi sasa haijatekelezwa.
Safari haikuishia hapo bali ikaendelea hadi katika kiwanda cha SAN FLAG pamoja na kiwanda cha chuma cha Lodhia ambapo Naibu Waziri amewataka wataalamu kutoka baraza la taifa la hifadhi na usimamizi wa mazingira kutoa tathmini za namna gani shughuli za uzalishaji unaharibu mazingira kiwandani hapo.
Kwa upande wao viongozi wa viwanda alivyotembelea Naibu Waziri Luhaga wameonekana wakijitetea kwa namna walivyopokea agizo kutoka serikalini hata hivyo msimamo wa serikali haujaweza kubadilika .
Ziara ya naibu waziri imefanyika ikiwa na lengo la kushiriki na wananchi wa Arusha katika kutekeleza siku ya usafi iliyotangazwa na serikali lakini pia ikiwa ni wiki ya usafi barani Afrika.
No comments:
Post a Comment