VIGOGO 10 wa kampuni ya Reli Tanzania (TRL) wanaokabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kukiuka sheria wakati wa ununuzi wa mabehewa 25, wameachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam.
Hakimu Mkazi Emilius Mchauru aliwaachia washitakiwa hao baada ya kutimiza masharti ya kuweka mahakamani Sh milioni 10, kuwa na wadhamini watatu waliosaini hati ya Sh milioni 10 pia wamewasilisha mahakamani hati zao za kusafiria na hawatakiwa kusafiri bila kibali cha mahakama.
Waliopata dhamana ni Mkurugenzi Mtendaji wa TRL, Kipallo Kisamfu, Mkuu wa Kitengo cha Makenika na Mhasibu Mkuu, Jasper Kisiraga; Kaimu Meneja wa Usafiri, Mathias Massae; Kaimu Mhandisi wa Ufundi na Meneja Ujenzi, Muungano Kaupunda na Mkuu wa Ufundi na Meneja Ujenzi, Ngoso Ngosomwiles.
Wengine ni Mhandisi Mkuu wa Ufundi, Paschal Mafikiri; Mhandisi Mipango Kedmo Mapunda; Kaimu Mhandisi wa Mawasiliano, Felix Kashaingili; Mkuu wa Usafiri wa Reli, Rowland Simtengu; na Kaimu Mkuu wa Usafirishaji; Charles Ndenge.
Hata hivyo, Mkuu wa Ubunifu na Utengenezaji wa Nyaraka, Joseph Syaizyagi bado yuko rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Februari mosi 2013 na Juni 30, 2014 katika Makao Makuu ya TRL, Kisamfu akiwa mfanyakazi wa mamlaka hiyo, alitumia vibaya madaraka yake kwa kushindwa kusimamia vizuri zabuni kama ilivyokuwa inatakiwa kwenye vigezo na masharti.
Inadaiwa jambo hilo ni kinyume cha Sheria Namba 21 ya Manunuzi ya 2004, jambo lililoipa faida Kampuni ya M/S Hindusthan Engineering and Industries Limited.
Ilidaiwa pia kati ya Julai mosi na Agosti 31, 2013, Mafikiri alitumia madaraka yake vibaya kwa kuidhinisha michoro iliyoandaliwa na M/S Hindusthan, jambo ambalo ni kinyume cha vigezo na masharti ya zabuni.
Kaunda anadaiwa alitumia madaraka vibaya kwa kuruhusu kutengenezwa kwa mabehewa 25, bila kuzingatia vigezo na masharti ya zabuni hiyo.
Katika mashitaka mengine Kisiraga na Massae, wanadaiwa walitumia madaraka vibaya kwa kuidhinisha malipo ya Dola za Marekani milioni 1.3 (sh bilioni 2.7) bila kuthibitisha matumizi ya mabehewa 25, kupitia Cheti cha Ukaguzi na cha kukubali kinachotolewa na TRL baada ya kufanyiwa majaribio