Thursday, February 11, 2016

WATUMIAJI WA BANDARI KUPIMWA ULEVI

KUANZIA Februari 15, mwaka huu, wafanyakazi na watumiaji wote wa Bandari ya Dar es Salaam watakuwa wanapimwa kiwango cha ulevi kabla ya kuingia, kuhakikisha kunakuwepo na mazingira salama ya kazi.
Meneja mawasiliano wa mamlaka ya bandari Tanzania(TPA) Janeth Ruzangi
Kwa mujibu wa wataalamu, kiwango cha kilevi kinachokubalika ni kile kizichozidi 0.5. Uamuzi huo ulitangazwa jana kupitia vyombo mbalimbali ya habari nchini na Kaimu Meneja Bandari hiyo, Hebel Mhanga aliyefafanua kuwa uamuzi huo umelenga kuboresha ufanisi wa watumishi.
Akizungumzia hatua hiyo, Meneja Mawasiliano wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Janeth Ruzangi alisema matumizi ya vilevi yanachangia kwa kiwango kikubwa utendaji kazi duni na kusababisha ajali mbalimbali kwenye maeneo ya kazi.
Ili kukabiliana na vitendo vya ulevi na dawa za kulevya, mamlaka hiyo kuanzia Jumatatu wiki iyajo kwenye milango yote (mageti) ya kuingilia bandarini kutakuwa na mashine za kupima kiwango cha kilevi kwa watumishi na watumiaji wote wa bandari hiyo.
Ruzangi alisema upimaji utafanywa nyakati zote za watumiaji hao kuingia bandarini na jambo hilo litakuwa la lazima kwa watumishi wote, na watakaobainika kuwa na kiwango cha kilevi kisichokubalika, hawataruhusiwa kuingia bandarini.
“Ni kweli utaratibu huo utaanza kutumika Februari 15, mwaka huu litakuwa zoezi endelevu na lengo lake ni kuimarisha masuala ya usalama na kuepusha ajali kwenye vyombo vya moto na mahali ya kazi katika eneo la bandari,” alifafanua Ruzangi.
Alisema kwa watumishi watakaobainika kuwa na kiwango cha kilevi kilichozidi 0.5 watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa sababu Kanuni na Sheria za kazi haziruhusu masuala ya ulevi maeneo ya kazi.
“Bandarini kazi ni nyingi na zinahitaji umakini kwa sababu kuna makontena, magari na bahari sasa kama umelewa unaweza kusababisha ajali na hiyo haikubaliki kitaifa na kimataifa,” alisisitiza Ruzangi.
Aliongeza pia kwamba Wakala wa Usalama na Afya Mahali Pa Kazi (OSHA) unataka pia kipimo hicho kifanywe kwa watumishi na watumiaji wa bandari ili kuhakikisha usalama eneo hilo nyeti upo.

No comments:

Post a Comment