Monday, February 29, 2016

Kigogo wa Republican amkataa Trump


 
TrumpImage copyrightGetty
Image captionTrump ametuhumiwa kwa kuwagawanya Wamarekani
Seneta wa Nebraska Ben Sasse amesema hatamuunga mkono mgombea urais anayengoza miongoni mwa wagombea wa chama cha Republican Donald Trump.
Sasse ndiye mwachama wa kwanza wa ngazi ya juu wa chama cha Republican aliyechaguliwa kutangaza hadharani kwamba hatamuunga mkono Trump.
Amesema amesikitishwa sana na kuvunjwa moyo na mfanyabiashara huyo na kwamba atamtafuta mgombea mwingine wa kumuunga mkono iwapo Trump atashinda uteuzi wa Republican.
Bw Trump tayari ameshinda uchaguzi wa mchujo katika majimbo matatu kati ya manne yaliyofanya mchujo kufikia sasa.
Aidha, anaongoza kwenye kura za maoni katika majimbo 11 ambayo yatapiga kura ya mchujo Jumanne.
Uchaguzi wa leo wa mchujo ambao hufanya siku hii kujulikana kama “Jumanne Kuu” huwa muhimu sana kwa wagombea kwani huamua wale walio na nafasi ya kushinda na wale wasio na uwezekano wa kushinda.
"Iwapo Donald Trump atakuwa mgombea wa Republican, nitamtafuta mgombea mwingine, mhafidhina au anayetetea katiba,” Seneta Sasse amesema kwenye ujumbe aliopakia katika ukurasa wake wa Facebook.
"Bw Trump ameangazia sana kuwagawanya Wamarekani, na kubomoa badala ya kujenga taifa hili tukufu,” ameongeza.
Bw Sasse, ni mwanachama mhafidhina katika chama cha Republican. Bado hajatangaza kuunga mkono mgombea yeyote kati ya wanaopambana na Bw Trump, lakini amepigia debe Marco Rubio na Ted Cruz.
Donald Trump amegawanya wengi hasa kwa matamshi yake ambayo yamekuwa yakizua utata.
Moja ya haya ni pendekezo lake la kujenga ua mpaka wa Mexico na Marekani ili kuzuia wahamiaji kuingia Marekani.
Aidha, mwishoni mwa mwaka uliopita, alipendekeza Waislamu wazuiwe kuingia nchini Marekani.

No comments:

Post a Comment