Wednesday, February 24, 2016

MADEREVA WA DALADALA ARUSHA WAGOMA.

Wakazi wa baadhi ya vitongoji vya jiji la Arusha wamekosa huduma ya usafiri baada ya watoa huduma ya daladala kugoma kwa madai ya kutaka barabara inayotoka katikati ya jiji kupitia Uswahilini Unga Limited kuelekea Muliet ikarabatiwe ili kuepusha ajali.
Madereva wanaotumia barabara hiyo wameeleza kuwa ubovu wake umekuwa ni kero ya siku nyingi hali inayochangia uharibifu wa magari na vyombo vingine vinavyotumia barabara hiyo.
Barabara inayolalamikiwa ni ya kutoka katikati ya jiji kupitia eneo la Uswahilini Unga limited kuelekea Muriet ambapo madereva hao wa daladala wanadai kuchoshwa na ubovu wa barabara hiyo inayodaiwa kuwa ni muhimu hasa kwa wakazi wanaoishi kandokando ya mji.
Akizungumza ofisini kwake mkurugenzi wa jiji la Arusha Juma Idd amesema barabara inayolalamikiwa pamoja na nyingine zinazotoka katikati ya jiji  ni miongoni wa barabara zilizopo katika mpango wa serikali wa kuimarisha barabara mkoani hapo  unaotegemewa kuanza hivi karibuni.
Mvua zinazoanza kunyesha mkoani Arusha zinapelekea uharibifu wa barabara kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu imara ya kupitisha maji yanayotokana na mvua.

No comments:

Post a Comment